HomeTanzaniaWasomi watoa maoni kuhusu EPA

Wasomi watoa maoni kuhusu EPA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wasomi watoa maoni kuhusu EPA

Dodoma, 12 Aprili, 2019.

Tanzania imeshauriwa kufanya tathmini ya kina kuhusu faida na hasara za kusaini Mkataba wa Ubia wa kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU) unaojulikana kwa kifupi EPA.Ushauri huo umetolewa na mbobezi wa masuala ya uchumi na mtangamano wa kikanda kutoka Ujerumani, Prof. Helmut Asche, alipokuwa anatoa muhadhara kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kuhusu changamoto za kutekeleza Mkataba wa EPA. Muhadhara huo umeratibiwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na UDOM ulifanyika tarehe 12 Aprili, 2019.

Prof. Asche alieleza kuwa, kutokana na kiwango cha uchumi wa Tanzania, Serikali itakuwa katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi ukizingatia kuwa nchi haiwezi kujitenga na biashara za kimataifa kutokana na umuhimu wake, ingawa kwa upande mwingine, zina gharama zake.

Prof. Asche alihitimisha muhadhara wake kwa kuitaka Serikali ya Tanzania kulishughulikia suala hili kwa umakini mkubwa huku ikizingatia hoja zifuatazo ambazo ni faida au madhara yatakayotokea endapo Tanzania itasaini au kutosaini Mkataba wa EPA; na hatua za kuchukua ili nchi zote za EAC zishawishike kusaini mkataba huo.

Akichangia mjadala huo, mtaalam wa uchumi na kilimo, Prof. Adam Mwakalobo, alieleza kuwa, kabla ya nchi haijachukua uamuzi wa kusaini Mkataba huo, kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa kina ili kujua faida na hasara nchi inazoweza kupata. Alisema nchi inaweza kuingia katika mkataba huo hatua kwa hatua na pasipo kuwa na hofu kwa kuwa nchi nyingine za Asia ambazo leo zimepiga hatua kubwa ya maendeleo, zilisaini mikataba kama hiyo kwa awamu.

Mchangiaji mwingine katika mada hiyo, Dkt. Cyril Chami, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, katika Serikali ya Awamu ya Nne, alibainisha masuala kadhaa ambayo yachukuliwe kama tahadhari kwa timu ya wataalamu inayofanya majadiliano ya mkataba huo.

Masuala hayo yamejikita katika utofauti mkubwa wa uchumi wa nchi za EAC na EU katika maneno ya pato la wastani kwa mtu mmoja (per capita income), wastani wa ukubwa wa uchumi wa jumuiya hizo mbili katika uchumi wa dunia kwa jumla, wastani wa bidhaa nchi za EAC inazouza EU na zile inazonunua, kiwango cha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchi za EAC na EU, maendeleo ya viwanda na pato linalotokana na ushuru wa forodha.

Kwa upande wake, Dkt. Godfrey Sansa, alisisitiza umuhimu wa kufanya majadiliano kwenye vipengele vya mkataba ambavyo nchi za EAC zina mashaka navyo kwa lengo la kupata  muafaka pasipo kuwekeana ukomo wa muda. Aidha, alisema kwenye mkataba kuwepo na kipengele cha kuruhusu kupitia upya mkataba huo kila baada ya muda fulani, kwa vile vipengele ambavyo utekelezaji wake vimeonekana vina madhara kwa nchi.
 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
 

Source

Stay Connected
255FansLike
473FollowersFollow
Must Read
Related News